Thursday, September 13, 2018
Wabunge waombwa kuunga mkono kazi za wasaidizi wa kisheria
Meneja Mradi wa Legal Services Facility LSF, Ramadhan Masele (kushoto), akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba wakati wa kikao chakujadili namna watakavyoweza kushirikiana na serikali namna ya kuboresha na kurahisisha upatikanaji wa huduma na msaada wa kisheria kwa wananchi hafla hiyo imefanyika jana jijini Dodoma.
Meneja Mradi wa Legal Services Facility LSF, Ramadhan Masele, akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Wabunge Tanzania wameombwa kuunga mkono kazi za wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada wa kisheria, ambao ni nguzo muhimu katika kuwasaidia mamilioni ya Watanzania kutoka katika vitendo vya kikatili, manyanyaso na udhalimu.
“Ni kweli kwamba wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada wa kisheria wengine wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaoteswa na kunyayaswa, lakini hawawezi kazi hii kwa ufanisi bila kusaidiwa au kuungwa mkono na watu kama vile wabunge,” Ramadhani Masele, Meneja wa Programu wa Taasisi ya Msaada wa Kisheria (LSF) wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku mbili kwa wabunge kuhusu wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za kisheria nchini, uliofanyika Dodoma jana.
LSF ni shirika lisilokuwa la kiserikali lilioanzishwa Mwaka 2011, linalofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DfID). LSF inatoa fedha kwa mashirika mbalimbali yanayotoa msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria Tanzania Bara na Zanzibar.
Lengo kuu la semina ya wabunge, ni kuwawezesha wabunge kujua masuala mbalimbali, ikiwemo namna wasaidizi wa kisheria wanavyotoa huduma zao, idadi ya wilaya wanazofanya kazi, na aina ya kesi wanazozishughulikia, msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria, kazi za LSF na ushiriki wake katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 17 ya Umoja wa Mataifana
Semina hii ya mafunzo inakuja wakati kuna ongezeko la matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu nchini, kama vile watu kuteswa, ukatili wa kijinsia, udhalilishaji wa kijinsia, kuwashambuliwa wanawake kwa kuwapiga, uporaji wa ardhi na matukio mengine yanayofanana na hayo.
Kwa kupatia ufadhili kutoka LSF, wasaidizi wa kisheria na watoa msaada wa kisheria wameweza kuwasaidia wanawake, wanaume na wasichana maskini na makundi ya watu wengine wananyimwa haki zao, kupata huduma za kisheria kwa gharama nafuu au bila gharama yoyote na huduma bora za msaada wa kisheria na hivyo kupata haki zao, kwa mujibu wa meneja Mpango wa LSF.
“Lakini wasaidizi wa kisheria na watoa msaada wa kisheria wengine wangeweza kutoa huduma na kuwafikia watu wengi zaidi ambao haki zimeminywa au kuvunjwa kama wakiungwa mkono na wabunge,” aliongeza Masele, huku akisema kwamba “wanawake na wanaume wanaoteswa, kudhalilishwa au kufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambao haki zao za ardhi na mirathi zimevunjwa, wanaishi katika majimbo yanayoongozwa na wabunge wenyewe.”
Pamoja na mambo mengine, alisema semina ya mafunzo itawasaidia wabunge kufahamu masuala yanayohusu wasaidizi wa kisheria, jinsi wanavyofanya shughuli zao na jinsi gani wasaidizi wa kisheria wanavyoweza kushirikiana na wabunge kupanua wigo wa huduma za msaada wa kisheria.
“Lengo kuu kuwasaidia watanzania wengi wanaohitaji msaada wa kisheria na kupata haki zao zilizokiukwa. Ni muhimu kwa wabunge kuungana na wasaidizi wa kisheria kwa sababu wananchi wenye matatizo wanatoka katika majimbo yanayoongozwa na wabunge,” alisisitiza Masele.
Kwa mujibu wa maelezo ya LSF, semina hii itawawezesha wa bunge kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na wasaidizi wa kisheria, ambao kwa sasa wanafanya kazi katika wilaya 170 nchini, namna ya kuwasiliana nao, namna ya kupata huduma zao na kueneza taarifa za huduma zao majimboni kwao.
“Taarifa muhimu kama hizi zitarahisha kazi za wabunge na wasaidizi wa kisheria katika kutatua matatizo/kero mbalimbali za wananchi katika majimbo yao—migogoro ya ardhi, ndoa na mimba za utotoni, mirathi, wanaume kutelekeza familia zao nk,” inasema sehemu ya taarifaya LSF.
Mada za kimkakati zilitolewa na wataalamu wa LSF kwenye semina iliyohudhuriwa na wabunge kutoka Kamati ya Kudumuya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment