Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Bw. Sisawo Konteh (Kulia) akishikana mikono na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Bw.Sabasaba Moshingi, wakati yeye na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo walipofika hospitalini hapo kujitolea damu kuadhimisha Siku ya Wachangiaji Damu Duniani, jijini Dar es Salaam Leo.
BENKI ya Biashara ya DCB imesema itaendelea kufanya jitihada tofauti katika kusaidia afya za watanzania wenye uhitaji wa kupata damu kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali imeelezwa jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza katika zoezi la kujitolea damu kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wachangia Damu Duniani, jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Bw. Sabasaba Moshingi alisema yeye pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzake wameamua kujitolea damu kwani licha ya benki yao kujishughulisha na utoaji wa huduma za kifedha lakini pia wanabeba jukumu la kuhakikisha watu wanaohitaji damu salama mahospitalini wanazipata bila kuwa na haja ya kusubiria ndugu waje kujitolea.
“Leo tupo hapa pamoja na washirika wenzetu hospitali ya Aga Khan kwa lengo la kuchangia damu, tutaendelea kushiriki matukio mengine kama haya na mengineyo yenye lengo la kusaidia kuokoa maisha ya watanzania wenzetu wenye uhitaji wa damu na mahitaji mengine ya kibidamu”, alisema Bw. Moshingi.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Kitengo cha Maabara katika Hosptali ya Aga Khan, Dk. Caroline Ngimba alitoa hamasa kwa watanzania wote nchini kuwa na moyo na utamaduni wa kujitolea damu bila kusubiri siku rasmi za kitaifa ama kimataifa bali liwe ni jambo endelevu kwani uhitaji wa damu upo kila siku mahospitalini.
“Uzuri ukichangia damu kama afya inaruhusu kila baada ya miezi mitatu unaweza kuchangia tena, tungeomba tabia hii iwe endelevu kwani hakuna kiwanda cha kutengeneza damu, damu inayopewa mwanadamu inatoka kwa mwanadamu”, alisema Dk. Caroline.
Naye mtaalamu wa utoaji damu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Peter Chami alitoa shukurani kwa Benki ya DCB, huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa benki hiyo ili kuokoa maisha ya watanzania wenye shida ya damu kwani mahitaji ya damu ni makubwa sana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Bw.Sabasaba Moshingi, akifanyiwa uchunguzi wa afya yake kabla hajajitolea damu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam leo, alipongoza baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo kujitolea damu, kuadhimisha Siku ya Wachangiaji Damu Duniani. Picha nyingine zikionesha matukio mbalimbali katika hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya DCB, Bw. Deogratius Thadei, akijitolea damu katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Wachangiaji Damu Duniani, katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam leo, ambako yeye pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzake walishiriki. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Maabara, Dk. Caroline Ngimba na kulia ni Mtaalamu wa mishipa Kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Bw. Peter Chami.
Baadhi ya wakurugenzi wa Benki ya DCB, waliojitolea damu pamoja na baadhi ya wafanyakazi wengine wa benki hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wachangia damu Duniani katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya DCB, wakishiriki zoezi la uchangiaji damu Ili kusaidia wenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wachangia damu Duniani, jijini Dar es Salaam leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya DCB, wakijitolea damu kusaidia wenye uhitaji ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wachangia damu Duniani, jijini Dar es Salaam leo.
No comments:
Post a Comment