Tuzo za ATE za Mwajiri Bora 2017 zazinduliwa jijini Dar - Serious Business

Mgongopr.blogspot.com is a serious online platform of business and finance news from around Tanzania. We are a trusted site covering the entire spectrum, from small enterprises to large businesses entities. For photography, videography, media management, events management, advertising, public relations, translation, interpreters, and more services, please contact us: MPP Ltd phone: +255 767765454, email: mgongo@gmail.com

Breaking

Monday, August 28, 2017

Tuzo za ATE za Mwajiri Bora 2017 zazinduliwa jijini Dar

 Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk.Aggrey Mlimuka (kulia), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa Tuzo za Mwajiri Bora (EYA) za mwaka 2017, zinatotarajiwa kutolewa baadae mwaka huu.Kushoto ni Joyce Nangai Ibengwe Mratibu wa tuzo hizo. 
oBaadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakihudhuria uzinduzi wa Tuzo za Mwajiri Bora za Mwaka 2017 jijini Dar es Salaam ambako Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dk. Aggrey Mlimuka (mbele, katikati) alizungumza nao.


HOTUBA ILIYOSOMWA NA DKT. AGGREY MLIMUKA, MKURUGENZI MTENDAJI WA CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA (ATE) SIKU YA UZINDUZI WA TUZO YA MWAJIRI BORA WA MWAKA 2017, IJUMAA TAREHE, 25 AGOSTI 2017, DAR ES SALAAM

 
Awali ya yote napenda kuwashukuru kwa kuja kujumuika na sisi asubuhi hii katika tukio hili muhimu sana katika kalenda ya Chama chetu. Lengo kuu la kukutana hapa ni kuwafamisha kuwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) leo tunazindua rasmi Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka 2017 ambayo pamoja na mambo mengine ni kutaka kutambua na kutoa tuzo kwa Waajiri wenye misingi bora ya usimamizi wa nguvu kazi na rasilimali watu  ili kuwawezesha kutimiza wajibu wao kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kibiashara.

Zoezi hili linalenga kuthamini mchango wa rasilimali watu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika utendaji wa masuala mbalimbali ya kibiashara. Tuzo ya mwajiri bora wa mwaka (EYA) ni zoezi lililoanzishwa na kuendeshwa kila mwaka na Chama cha Waajiri Tanzania tangu mwaka 2005.

Tuzo ya mwajiri bora wa mwaka inalenga zaidi kuwatambua wanachama waliofanya vizuri katika kuweka mikakati bora yenye kuthamini usimamizi wa rasilimali watu na shughuli za kibiashara. Kwa miaka kadhaa tuzo hizi zimehamasisha makampuni wanachama kuweka juhudi katika masuala ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu kama msingi mkakati wa makampuni yao kujenga nguvu kazi yenye ujuzi,furaha, ushindani, na yenye kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

Kutokana na maoni tuliyopokea kutoka kwa wanachama,wadau na wataalamu wetu mbalimbali, ninayo furaha kukujulisheni kuwa mwaka huu tuzo ya mwajiri bora itakuwa ya kipekee na ya kusisimua. Tumeongeza vigezo na vipengele vipya ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kibiashara. Baadhi ya vigezo vimeboreshwa na pia dodoso za upataji taarifa zimerahisihwa zaidi. Vigezo vipya vya tuzo hizi kwa mwaka 2017 zimejikita katika nyanja zifuatazo:-

·         Mwajiri bora anayejali uwiano wa kazi na maisha atatuzwa. Utafiti unaonesha kwamba utendaji bora unatokana na uwepo wa uwiano mzuri baina ya wasaa wa kazi na mapumziko. Waajiriwa wanapohamasishwa kujikita katika utendaji unaolenga matokeo ya kazi badala ya muda wanaopaswa kufanya kazi hujihisi kuthaminiwa sana na hivyo uzalishaji wao huongezeka maradufu.

·         Pia mabadiliko katika soko la ajira la Tanzania yametokana na mambo mbalimbali ilkiwemo kupungua kwa idadi ya wastaafu, changamoto za mafao, ukuaji wa sekta ya viwanda zalishi sambamba na ongezeko la wahitimu wapya vyuoni katika ngazi mbalimbali na hivyo Chama cha Waajiri Tanzania kinaamini kwamba mwajiri bora ni yule anayesimamia vema nguvu kazi inayoonekana kupotea/kupuuzwa na hivyo mwajiri huyo anafaa kupewa tuzo kwa jambo hilo ili nguvu kazi hiyo anayoisimamia iendelee kudumisha ubora wake wa kazi kwenye soko la ajira. Wazee wana faida nyingi ikiwemo suala la kupunguza gharama.

·         Waajiri bora wenye mikakati inayojali afya za waajiriwa. Lengo likiwa ni kuboresha hali ya afya za waajiriwa ili kukuza utendaji kazi na kuongeza morali ya kazi kwa waajiriwa.        

·         Waajiri bora ambao wameweza kusimamia dhana ya utofautishwaji na ushirikishwaji yaani (diversity and inclusion) kwa kuhakikisha kuwa panakuwepo na sera na mikakati ya kutosha ili  kuhakikisha usawa katika fursa za ajira haupo tu kwa watu wenye ulemavu bali kwa watu wote.

·         Waajiri bora waonaowachochea na kuwajali waajiriwa wenye ujuzi. Kuna waajiri ambao wamefanikiwa kuwabakiza waajiriwa wao kwa kuweka programu nzuri za kiutendaji na pia wameweza kuwavutia waajiriwa wapya na kuhakikisha hawaondoki kwenye makampuni yao..

·         Waajiri bora wenye mahusiano mazuri baina ya waajiri na waajiriwa na uendeshaji mzuri wa kazi ambao ni muhimu katika kujenga mazingira rafiki ya kazi. Maelewano ya kikazi na masuala ya ajira bado ni changamoto kwa waajiri wengi na hivyo hupelekea migogoro mingi. Masuala yahusuyo makubaliano ya pamoja (kati ya mwajiri na mwajiriwa), uhuru wa kujumuika pamoja na mikataba ya ajira yatapitiwa upya na kupewa tathmini.

·         Waajiri bora wenye majina makubwa na imara huvutia wateja, waajiriwa, wadau n.k. na mara nyingi ni waajiri wenye kupendwa zaidi. Kwa mwaka huu Chama cha Waajiri Tanzania kitatoa tuzo kwa waajiri bora ambao sifa yao ni ya kweli, kuaminika, yenye kusadifu na kuleta mafanikio.

·         Pia, Chama cha Waajiri Tanzania kitatoa tuzo kwa mwajiri bora aliyewekeza kwenye teknolojia. Makampuni ya kisasa yanawekeza kwa kasi katika matumizi na usimamizi wa teknolojia ili kuleta ushindani. (Competitive advantage).  Maana ya teknolojia mpya ni utumiaji wa maarifa, ujuzi, vifaa na mitambo ya kisasa katika kuzalisha bidhaa au kutolea huduma

Mkurugenzi Mtendaji alisema aliongeza kuwa vigezo vingine vya utoaji wa tuzo vitaendelea kujikita katika masuala ya utawala na uongozi, ubora katika usimamizi wa rasilimali watu, bidhaa au huduma, uzalishaji na ubunifu, uwajibikaji katika mwenendo wa biashara, utendaji unaokidhi, ushirikishwaji wa mwajiriwa, ukuzaji wa vipaji, mafunzo na maendeleo pamoja na usalama wa mwajiriwa katika mazingira ya kazi.

Chama cha Waajiri Tanzania pia kimetambulisha vipengele vitatu vya tuzo zitakazotolewa kwa kigezo cha upana wa mawanda ya uendeshaji wa kampuni. Kwa kuzingatia taratibu zilezile za usimamizi wa rasilimali watu ambazo ndio za msingi na za kimataifa kulingana na vigezo vilivyotumiwa na mtaalamu wa masuala ya ajira, tutakuwa na tuzo ya waajiri bora katika sekta binafsi, sekta za umma pamoja na mashirika ya ndani ya nchi. Kutokana na maoni ya wanachama wetu, kumekuwa na hisia kwamba kushindanisha makampuni yote kwa namna moja hakuleti usawa kwenye mashindano. Hii ni kwa sababu makampuni yanatofautiana kulingana na sekta yalizojikitika kiuendeshaji  na hivyo suala la utoaji  wa tuzo kwa kuzingatia na sekta husika ni muhimu kulingana na mahitaji, mienendo na matakwa au misingi mbalimbali ya umiliki.

Shughuli hii ina sehemu mbili; sehemu ya  kwanza ni ya utafiti itakayopelekea kupata washindi na kwa sasa sehemu hiyo ipo chini ya kampuni binafsi, TanzConsult inayoongozwa na Prof. BAT Kundi,  na sehemu ya pili ni usimamizi wa matukio mpaka kilele cha sherehe ambacho kimepangwa kuwa Ijumaa ya tarehe 8 Disemba 2017. Nawasihi wanachama wote kushiriki mashindano haya ili kupata fursa ya kulinganisha utendaji wa makampuni yao na ya wengine.

Nawasihi wanachama kutembelea tovuti yetu ya tuzo za waajiri ambayo ni www.eya2017.co.tz  ambayo itawaongoza mpaka kwenye dodoso lililoko mtandaoni. Makampuni shiriki yanaombwa kuwasilisha madodoso mawili yaliyojazwa, moja likiwa limejazwa na uongozi au mkurugenzi mkuu au mkuu  wa kitengo cha usimamizi wa rasilimali watu na dodoso jingine  lililojazwa na mwajiriwa wa kawaida au mwakilishi wa chama cha wafanyakazi. Mwaka huu pia Chama cha waajiri (ATE) kimeanzisha mwongozo wa habari juu ya tuzo za Waajiri (EYA Information Guide) ili kurahisisha ushiriki na uelewa juu ya zoezi hili muhimu.


Kuhusu Chama cha Waajiri Tanzania (ATE)

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ni chombo pekee cha waajiri kinachowawakilisha vema nchini Tanzania. Kiliundwa mwaka 1960 ili kusimamia na kulinda maslahi ya waajiri katika masuala ya kazi na ajira.

Kama sauti muhimu ya masuala ya kibiashara, Chama cha waajiri Tanzania kinawakilisha waajiri katika sekta zote zinazohusu uchumi wa taifa isipokuwa zile za utumishi wa umma. ATE ina jumla ya wanachama wa moja kwa moja wapatao 1400 waliosajiliwa na wengne wapatao 6000 wasio wa moja kwa moja wanaaotoka makampuni binafsi ya kibiashara na baadhi ya mashirika ya umma.
Nje ya mamlaka  yake kuu ya kulinda maslahi ya waajiri na kuhakikisha mahusiano mazuri baina ya waajiri na waajiriwa makazini, Chama cha Waajiri Tanzania kinahamasisha na kuchochea mienendo mizuri ya usimamizi wa rasilimali watu na misingi bora miongoni mwa waajiri ili kurahisisha uendeshaji wa biashara ambao ni muhimu katika uzalishaji na ushindani na hivyo huandaa tuzo  za waajiri kila mwaka ili kutambua na kuthamini makampuni yaliyofanya vema katika kulinda misingi na mienendo ya usimamizi wa rasilimali watu.
Chama hutoa uanachama unaojumuisha makampuni makubwa, ya kati, madogo na madogo zaidi kutoka sekta mbalimbali za uchumi wa taifa. Wanachama ni pamoja na makampuni binafsi na ya umma, mashirika ya umma, vyama vya ushirika, balozi mbalimbali, vyama vya kibiashara, taasisi za kidini, asasi binafsi (NGOs), na watu binafsi. Uanachama wa ATE upo kwa ajili ya waajiri wote nchini Tanznia:- watu binafsi,vikundi, makampuni, mashirika ya umma, serikali za mitaa na mamlaka zingine za nchi au vyama vya waajiri na kwa sasa chama kimegawanyika katika idara 8 ikiwemo kilimo, biashara, viwanda, ushirika na huduma, benki na fedha, madini, mafuta na usalama binafsi.

Kwa taarifa zaidi wasiliana na mratibu wa mradi wa tuzo za waajiri (EYA Project Coordinator) Joyce Nangai kupitia +255 784 702670 au barua pepe nangai@ate.or.tz au wasiliana na Afisa Mawasiliano (Communications Officer), Yunge Kanuda kupitia +255 657 453618 au barua pepe kanuda@ate.or.tz



No comments:

Post a Comment

Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu

Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...

Pages