Maria na Consolata wakiwa kidato cha sita mwaka 2017
"Maumbile ya Maria na Consolta ndio sababu kubwa iliyochangia kifo chao" Daktari Mseleto Nyakiloto ameeleza hayo alipozungumza na BBC.
Mseleto Nyakiloto ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji na mganga mfawidhi wa hospitali ya Iringa ameeleza chanzo kilichopelekea wasichana hao kufariki ni tatizo la njia ya hewa.
"Mmoja alitangulia na mwingine alifariki baada ya dakika kumi,Maria ndio alikuwa ana tatizo la kiafya kwa kuwa mapafu yake yalishindwa kufanya kazi na huyu mwingine alikufa kutokana na viungo vingi katika mwili wao wanavitumia kwa pamoja".Dr.Nyakiloto aeleza.
Hata hivyo daktari huyo aliongeza kwa kusema kwamba mzunguko wa hewa na damu ndio umesababisha kifo cha cha mwingine hivyo matarajio ya mmoja kupona yasingewezekana.
Maria na Consolata walikuwa wakitumia kwa pamoja baadhi ya viungo vyao.
Aidha daktari Nyakiloto amesema mapacha wa aina hii wapo wa aina nyingi ingawa muda wa maisha yao huwa unatofautina kutokana mazingira pia; kuna wale ambao hata hawafikii hatua ya kuzaliwa,wengine wanakaa muda mfupi wanafariki na wengine ndio wanajitahidi wanafikia umri mkubwa kama ya kina Maria na Consolata wameweza kufika miaka 21.
Maria na Consolata walipokuwa na miaka sita
Mwaka 2004,BBC iliandika juu ya watoto hawa mapacha ambao walikuwa na miaka sita kuwa maisha yao yako kwenye mashaka.
Tatizo kubwa ambalo lilikuwa linawasumbua ilikuwa mapafu yao yana uzito mkubwa kuliko mwili wao.
Madaktari walikuwa na hofu juu ya tatizo la mmoja linaweza kusababisha mwingine kuathirika na kuwafanyia upasuaji,kutaongeza tatizo kuwa kubwa zaidi.
Maria aliwahi kula kwa ajili ya mwenzake kwa miaka mitano.
Miguu yao ilikuwa sehemu kubwa ya mwili wa Maria na Consolata
Miguu yao ilikuwa imechukua sehemu kubwa ya mwili.
Kwa Maria mguu wake wa kulia ndio ulikuwa na nguvu wakati Consolatha ulikuwa wa kushoto na miguu yao mengine ilikuwa haifanyi kazi.
Walikuwa na vichwa viwili,mioyo miwili na mikono minne.
Na walikuwa wanatumia viongo vingine kwa pamoja kama tumbo,ini,sehemu ya uke na haja.
Maria alikuwa na matatizo ya kiafya tangu alipozaliwa, alikuwa na shida ya kupumua ingawa licha ya kuwa alikuwa ana uwezo wa kula chakula zaidi ya mwenzie.
Maria alikuwa akila kwa niaba ya ndugu yake kwa takribani miaka mitano na nusu ndipo Consolata na yeye alipoanza kula mwenyewe.
Wanatumia baadhi ya viungo kwa pamoja
Dr Rainer Brandl aliiambia BBC Network Africa mwaka 2004, kuwa mapafu yao yalikuwa hayako sawa kwa namna ambayo hawawezi kuimili miili yao na hayawezi kuongezeka zaidi.
Na kilichobaki ni kuwaombea ili waendelee kuishi kwa matumaini.
Katika maisha yao kutegemeana ndio jambo la kubwa na kawaida katika maisha yao, kwa mfano Maria akitaka kwenda chooni atamjulisha mwenzie na vivyo hivyo kwa Consolata.
Maisha yao yalijawa na ndoto nyingi.
Maria na Consolata wakiwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli
Maria na Consolata walikuwa ni walikuwa katika maisha yenye matumani na walitamani siku moja kuwa walimu na waliweza kuingia chuo kikuu kusomea masomo ya ualimu.
Licha ya kuwa zamani walikuwa ndoto tofauti lakini baadae waliweza kuwa na nia moja ya kuwa walimu.
Walikuwa wanatofautiana pia katika tabia,fikra na hata kuongea.
Awali mmoja alipenda kuwa daktari na mwingine kuwa sista lakini badae wote wakapenda kuwa walimu.
Kazi ya ualimu ilikuwa ndoto ya Maria na Consolata
Wanapenda vitu tofauti pia kuna ambaye alikuwa anapenda muziki wa bongo fleva na mwingine injili.
Watoto hao pia walikuwa wanagombana na kupatana.
Maisha yao yalikuwa ya neema kutokana na mazingira waliyokulia na wanafunzi wenzao waliona kuwa watoto hao walikuwa chachu katika jamii kutowatenga watoto walemavu.
Ndoto yao kuwa pia ambayo waliibainisha walipozungumza na BBC ni kwamba walikuwa wanamatumaini ya kuolewa na mume mwerevu na watayeweza kumsaidia na asione kuwa wao ni tegemezi.
Mapacha walioungana wakoje?
Mapacha walioungana huwa ni wachache sana kutokea au kuwepo, katika watoto laki mbili wanaozaliwa kila mwaka anazaliwa mtoto mmoja tu wa aina hiyo.
Watoto wengi huwa hawawezi kuishi ,hufa mara baada ya kuzaliwa au mimba huharibika.
Watoto hawa uzaliwa katika uzao wa yai moja,hufanana na wana jinsia moja.
Kuzaliwa kwa watoto hawa huwa kuna hali ya kustaajabisha,kwa ujumla Watoto hao wanaweza kuishi wakizaliwa katika hali hiyo huwa ni kati ya asilimia 5 mpaka asilimia 25.
Katika rikodi za historia zinasema kwamba mapacha wa kuungana wengi wanaoweza kuishi kwa muda mrefu ni wa kike,kwa asilimia 70
Mapacha walioungana wamegawanyika katika sehemu tatu
•73% wameunganika kuanzia kwenye kifua na tumbo
•23% wanakuwa wameunganika katika sehemu ya chini ya mapaja na miguu
•4% wanakuwa wameunganika kichwa
Mapacha walioungana waliowahi kuwa maarufu duniani
Mapacha Eng na Chang
Kwa miaka mingi mapacha walioungana wameendelea kuishi kutokana na matokeo ya tafiti nyingi zilizofanywa na majaribio mengi ya upasuaji yaliyofanyika.
Mapacha wa kwanza wa kuungana waliojipatia umaarufu mkubwa duniani walijulikana kama 'siamese' majina yao yalikuwa ni Eng na Chang.
Mapacha hao walizaliwa mwaka 1811 waliweza kuishi kwa miaka 63 na kufanikiwa kupata watoto 22 kutoka kwa wadada wawili ndugu waliowaoa wakiwa na umri wa miaka 21, Chang alikuwa na watoto 12 na Eng watoto 10.
Walipozaliwa jamii ilitaka kuwauwa lakini kwa kudhaniwa kuwa wataleta mikosi na walioneka kuwa nio viumbe wa ajabu.
Mapacha wa kuungana na maisha yao ya ndoa
Katika karne ya ishirini,mapacha wa kuungana walikuwa wanazuiwa kuoa au kuolewa nchini Marekani.
Na hii iliibua hisia za wengi pale ambapo wanamuziki ambao ni wacheza filamu wa nchi hiyo Daisy na Violet walipotaka kuolewa.
Daisy na Violet mapacha waliokuwa wacheza filamu.
Watu wengi waliwaona kuwa maumbile yao hayawezi kuwaruhusu kuolewa au kupata wenza ingawa mapacha wenyewe wanajiona wamekamilika.
Kwa upande wa Chang na Eng ambao walifanikiwa kuoa, maisha yao ya ndoa yalikuwa na changamoto nyingi hasa pale ambapo wake zao walipoanza kugombana na kupelekea wake hao kuishi kwenye nyumba mbili tofauti.
Kwa maisha yao yote mapacha hao walikuwa wanaishi kwa mke mmoja siku tatu na mwingine siku tatu.
Vilevile mapacha kutoka Tanzania, Consolata na Maria ndoto yao kubwa baada ya shule ni kuolewa na mume mmoja.
No comments:
Post a Comment