Saturday, August 31, 2019
Bibi kizee arudishiwa ardhi iliyochukuliwa na mwenye pesa Korogwe Tanga
Bibi kizee na Mkazi wa Korogwe, Bi. Amina Kirua, akilima katika shamba lake alilonyang’wa na jirani yake Tajiri, lakini baadae alirudishiwa baada ya kusaidiwa na wasaidizi wa kisheria Wilayani Korogwe. Msaada huo ni sehemu ya mradi mkubwa na nchi nzima wa kuwawezesha watanzania maskini na wahitaji, unaofadhiliwa na shirika la Legal Services Facility (LSF). (Picha na Mpiga Picha Wetu).
Tanzania inakumbana na changamoto nyingi zinazohusiana na umilikaji wa ardhi, hasa sehemu za vijijini. Changamoto hizi ni pamoja na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, migogoro ihusuyo muda wa umiliki wa ardhi, uporaji wa ardhi na wakulima kunyang’anywa ardhi. Waathirika wakubwa wa migogoro ya aina hii ya ardhi ni wanawake na wazee waishio vijijini,” anasema mtaalamu wa masuala ya ardhi Charity Mugabi katika utafiti wa hivi karibuni na kuongeza: “Sera ya Ardhi tuliyo nayo kwa sasa na utekelezaji wake havijaweza kutatua migogoro ya ardhi nchini.”
Bibi Amina Kirua alikuwa akimiliki ekari 6 katika Wilaya ya Korogwe Vijijini Mkoa wa Tanga. Alinunua ekari hizo sita takriban miaka 25 iliyopita kutoka kwa jirani yake, ambaye ameshafariki dunia. Bibi huyu anaishi peke yake, lakini ana watoto wawili wa baba tofauti.
Ni bibi maskini anayetegemea shamba lake linalomsaidia kupata kipato cha kuendeshea maisha yake na watoto wake Hassan Bembe na Musoli Jumbe, ambaye huyu wa pili ana matatizo ya akili. Kwa miaka mingi, Bibi Amina amekuwa akilima kwa kujikimu na wanakijiji wengi katika Wilaya ya Korogwe Vijini.
Wakati fulani mtoto wake mwenye matatizo ya akili alihitaji uangalizi wa karibu kwa sababu ya matatizo ya kiafya. Hali hiyo ilimfanya Bibi Amina atumie muda wake mwingi kumtunza mtoto wake. Hivyo, aliacha kulima kama alivyokuwa akifanya kwa zaidi ya miezi miwili ili amtunze mtoto wake.
Baada ya mtoto wake kupata nafuu, alienda shambani kwa lengo la kuendelea na shughuli zake za kilimo. Lakini hakuamini alipokuta jirani yake ambaye ana uwezo wa kifedha akilima shamba hilo kwa madai kwamba yeye ndie mumiliki halali wa shamba hilo. Hivyo, mgogoro wa ardhi ulianza kati ya majirani hao, huku yule mwenye uwezo wa pesa akitumia uwezo wake wa pesa kuwahonga watendaji ili kumnyang’anya Bibi Amina ardhi, ambaye ni mumiliki halali, na kupewa yeye na hivyo kumfanya Bibi Amina kupoteza haki yake ya kumiliki ardhi.
Wanakijiji wenzake walimshauri Bibi Amina kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza la Kata Korogwe Vijijini. Kutokana na nguvu ya pesa, Baraza la Kata liliamua kuwa ardhi ni mali ya yule mwenye pesa na hivyo Bibi Amina akapoteza haki yake.
“Kutokana na uamuzi wa Baraza la Kata, nilipoteza umiliki wa ardhi, lakini sikukata tamaa kwa sababu nilijua kwamba ardhi hiyo ni mali yangu, kwani niliinunua kwa pesa yangu mwenyewe,” alisema Bibi Amina. Kwa kweli, alikuwa ndiye mumiliki halali wa ardhi hiyo, lakini hakuwa na jinsi kutokana na uamuzi huo wa Baraza la Kata.
Watendaji walewale waliopokea pesa kutoka kwa jirani yake Bibi Amina na kumpokonya ardhi Bibi Amina walienda kwake kwa siri kumshauri aende kumwona msaidizi wa kisheria wa Wilaya ya Korogwe Vijijini Maimuna Hosean kwa msaada zaidi.
Wasaidizi wa kisheria walimsaidia Bibi Amina kuandaa hati, ushahidi na kukata rufaa kwenda Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Korogwe Mjini. Baada ya kusikiliza shauri lake, Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya lilitoa uamuzi kwamba yeye ndiye mumiliki halali wa ardhi hiyo.
“Kuanzia hapo, yule jirani yake aliyetumia nguvu ya pesa kumnayang’anya ardhi alishindwa kesi na hadi leo hajambugudhi tena Bibi Amina kuhusu umiliki wake wa ardhi,” alisema Yahaya Seif, ambaye ni msaidizi wa kisheria aliyeongoza wasaidizi wa kisheria wenzake kumtetea Bibi Amina kupata haki yake ya kumiliki ardhi kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.
“Huduma za msaada wa kisheria hazina budi kuwafikia wanaume na wanawake wazee wanaokabiliwa na migogoro ya ardhi kutokana na uzee, umaskini na kutojua kusoma na kuandika sehemu mbalimbali za Tanzania vijijini,” alisema kiongozi mmoja, ambaye ni jirani wa Bibi Amina.
“Migogoro ya ardhi kama huu siyo mipya sehemu mbalimbali za Bara la Afrika… watu wachache wenye uwezo wa pesa na uchu wa kujilimbikizia mali hawaridhiki na walichonacho. Wanataka wachukue hata sehemu ndogo ya ardhi ambayo inamilikiwa na maskini. Hatua za kisheria lazima zichukuliwe kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kuwalinda wanaume na wanawake maskini dhidi ya unyanganyaji wa ardhi,” alisema mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu, Bw Ramadhan Mweli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania Yakamilisha Kampeni ya Kusisimua ya "Spend & Win" kwa Droo ya Mwisho na Hafla ya Kukabidhi Gari
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Lilian Swere (kushoto), akihutubia hadhira wakati wa droo ya tatu y...
No comments:
Post a Comment