Friday, January 31, 2020

DCB YATENGENEZA FAIDA YA SHILINGI BILIONI 2.3 MWAKA 2019
Mkurugenzi wa Fedha
wa Benki ya Biashara ya DCB, Zacharia Kapama (wa pili kushoto), akisoma hotuba
yake katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo
wakati wa kutangaza taarifa za fedha ambapo alisema DCB imepata faida ya
shs bilioni 2.3 kwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 43 kutoka faida ya
mwaka 2018 ambayo ilikuwa shs bilioni 1.6. Wengine kutoka kushoto ni;
Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano, Rahma Ngassa, Mkurugenzi wa Biashara,
James Ngaluko na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Fortunata Benedict, wote
kutoka DCB.
Benki ya biashara ya DCB (DCB
Commercial Bank Plc) imetangaza kupata faida ya shilingi bilioni 2.3 katika
mwaka 2019, ikiwakilisha ongezeko la asilimia 43 kutoka faida ya mwaka
2018 ambayo ilikuwa shilingi bilioni 1.6
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo
mbalimbali vya habari leo tarehe 31 Januari 2020 na iliyochapishwa katika
magazeti kwa mujibu wa sharia za benki kuu, utendaji wa benki umeendelea kuimarika
ikilinganishwa na mwaka uliotangulia huku ufanisi katika nyanja zote muhimu
ukiongezeka kwa kiwango cha kuridhisha.
Akiwakilisha taarifa za fedha za robo
ya nne ya mwaka 2019, mkurugenzi wa Fedha wa benki ya DCB Ndugu Zacharia
Kapama, ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na ukuaji wa mizania ya benki,
ambao umechagizwa na ukuaji wa amana za wateja kwa asilimia 14 (Shilingi
bilioni 10.1), ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Ukuaji wa amana umeisaidia benki pia
kuongeza ukuaji wa mikopo ambapo benki imefanikiwa kuongeza kiwango ghafi cha
mikopo kwa asilimia 11 (shilingi bilioni 8.0), ambacho ni kiasi kikubwa
ukilinganisha na ongezeko la mikopo katika miaka miwili iliyotangulia. Mikopo
ghafi ya benki imekua kutoka shilingi bilioni 90.5 mwaka 2018
kufikia shilingi bilioni 93.3 mwaka 2019.
Ili kufikia kiwango hiki, benki
imefanikiwa kutoa mikopo mipya kwa wateja wake kinachofikia shilingi bilioni
60, huku shilingi bilioni 18 zikiwakilisha mikopo kwa wafanyabiashara
wadogo na wa kati (SMEs), na Shilingi Billioni 10 ikiwakilisha mikopo ya wanawake
na vijana. Benki pia imeendelea kutoa mikopo kwa sekta mbalimbali zikiwemo
sekta binafsi za biashara, elimu afya na ujenzi.
Akielezea upatikanaji wa faida, Ndugu
Kapama ameainisha kuwa ukuaji wa faida, ukiachilia mbali kuchangiwa na ukuaji
wa mizania, pia umechagizwa na ongezeko la mapato yasiyotokana na riba baada ya
benki kufanikiwa kukuza idadi ya wateja wake kutoka 175,000 mwaka 2018 kufikia
wateja 194,000 mwaka 2020. Ongezeko hili limeongeza idadi ya akaunti za amana
na miamala ya kibenki, huku wateja wakifurahia huduma za kidijitali bila kwenda
matawini.
Kwa kuongezea, ufanisi wa benki
umeongezeka hasa katika usimamizi wa matumizi ya riba na yasiyo ya riba. Benki
imefanikiwa kudhibiti ukuaji wa matumizi yasiyo ya riba, huku ikihakikisha
huduma kwa wateja zinaboreshwa. Benki pia imefanikiwa kudhibiti ongezeko la
riba kwa wateja na kuhakikisha wateja wanapata thamani bora ya huduma zake bila
kuathiri ukuaji wake.
Katika taarifa hiyo, Ndugu Kapama pia
ameainisha upunguaji wa mikopo chechefu ya wateja kutoka asilimia 19 mwaka 2018
kufikia asilimia 13 mwaka 2019. Hii imetokana na juhudi za benki kuhakikisha
kuna ufanisi na usimamizi madhubuti katika utoaji mikopo na ukusanyaji madeni. Benki
itaendelea na juhudi za kuhakikisha mikopo chechefu inafikia kiwango
kinachokubalika na wadau wa sekta ya fedha mnamo mwaka huu wa 2020.
Katika miaka yake takriban 17 ya
uendeshaji, benki ya DCB imeweza kukuza idadi ya matawi kutoka tawi moja na
kufikia manane (8) hadi mwaka huu wa 2019. Pia imekuza idadi ya wateja kufikia
194,000. Ukuaji huu umechangia benki kupata faida mfululizo tangu mwaka 2004
hadi mwaka 2015, na imekuwa ikitoa gawio kwa wanahisa wake katika kipindi chote
cha miaka 12.
Hapo mbeleni, benki ya DCB, inatazamia
kukuza mizania yake kwa kutumia fursa za ukuzaji biashara na ina azimia kutumia
ipasavyo fursa na njia mbadala za utoaji huduma kwa wateja kupitia mitandao,
wakala wa kibenki, na upanuzi wa mitandao ya matawi na vituo vidogo vya huduma ambapo
itasaidia kwa kiasi kikubwa utengenezaji wa mapato kupitia njia ya mapato yasiyo
ya riba.
Benki ya DCB ndio benki ya kwanza
kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam huku ikiwa ndio benki pekee
iliyokua kutoka benki ya wananchi/jamii (community bank) na kufanikiwa kuwa
benki ya biashara (commercial bank).
Benki ya DCB imefanikiwa kukuza
mtandao wa matawi yake kufikia manane huku ikifungua tawi Dodoma na inaendelea
na mchakato wa kufungua matawi na vituo vya huduma (service centers) katika
mikoa mingine na imefungua mtandao wa mawakala na huduma za kijiditali hadi
kufikia mawakala zaidi ya 700 nchini nzima.
Benki imefanikiwa kuongeza mtaji wake
kupitia soko la hisa kwa miaka yote 18 huku ikipata faida mfululizo na
kujiimarisha kibiashara. Hivi sasa benki inao uwezo wa kutoa mikopo mikubwa
zaidi na ya muda mrefu kwa wateja.
Benki imefanikiwa kuzindua mfumo wa
akaunti za kidijitali ambapo umeiwezesha kuhudumia wateja wengi zaidi na
kuwafikia hadi wale wa vijijini. Hii imeongeza ukuaji wa mapato na ongezeko la
idadi ya wateja na ufanisi katika utoaji huduma.
Akielezea maboresho zaidi ya huduma za
kibenki yaliyofanyika, Mkurugenzi wa biashara Mr James Ngaluko alieleza:
Benki imefanikiwa kuzindua huduma na
bidhaa mpya kwa wateja wake ambazo ni Lamba kwanza (Fixed deposit), Akaunti ya
Skonga, DCB sokoni, pamoja na garantii za wakandarasi zisizo na dhamana wakati
wa kuomba tenda.
Tumeboresha huduma ya mikopo ya nyumba
ujenzi wa nyumba kwa kuongeza ushirikiano na Tanzania Mortgage Refinancing
Company.
Tumeongeza ufanisi wa huduma ya mikopo
kwa ushirikiano na taasisi ya ushauri
FSDT, hivyo kufanya huduma ya utoaji mikopo kwa wateja kuwa ya haraka Zaidi.
Benki imeboresha gharama zake kwa
kuondoa gharama katika akaunti za community kama vikoba, akaunti za miradi ya
serikali, na akaunti za wastaafu. Hii imepelekea kuongeza idadi kubwa ya wateja
ambao wengi ni wa kipato cha cha chini na cha kati.
Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa
mwaka 2002 (Ikijulikana kama Dar es Salaam Community Bank) kutokana na kilio cha wakazi wengi wa jiji la
Dar es Salaam kutokuwa na namna ya kupata mitaji midogo ya biashara jambo
ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwa wajasiriamali wadogo wadogo katika
jitihada za kuboresha biashara zao sambamba na masharti magumu kutoka kwa benki
nyingi za kibiashara. Kwa kipindi chote cha miaka 17 ya uendeshaji, jukumu mama
la benki hii limeendelea kuwa ni kutoa huduma bora za kifedha huku ikijikita
zaidi katika kutengeneza miradi endelevu ya kupunguza umaskini na kuendeleza
jamii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya wanawake mahali pa kazi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Kikwete (kushoto), akikabidhi cheti Kwa Mkurugenz...

No comments:
Post a Comment