Saturday, August 15, 2020
SENSA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI CHACHU YA MAENDELEO YA VIWANDA-DKT.CHUWA
Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akisisitiza umuhimu wa sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa viongozi na wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Isangha wilayani Bahi mkoani Dodoma wakati alipotembelea Kijiji hicho kujionea utendaji wa wadadisi wa sensa hiyo.
Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akisisitiza jambo kwa mkazi wa Kijiji cha Isangha wilayani Bahi mkoani Dodoma Bw. Robert Maswaga wakati alipotembelea Kijiji hicho kujionea utendaji wa wadadisi wa sensa hiyo.
Mtakwimu mkuu wa Serikali Dkt. Alibina Chuwa akiwapongeza na kuwaelekeza jambo
wadadisi wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika kijiji cha Isangha wilayani Bahi wakati wa ziara yake iliyolenga kuona utendaji wao.
Sehemu ya mifugo iliyokutwa katika moja ya Kaya zilizochaguliwa kushiriki katika sense ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kama ilivyokutwa katika kijiji cha Isangha wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Wadadisi wa Sensa ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakijadiliana jambo katika kijiji cha Isangha wilayani Bahi mkoani Dodoma wakati wa ziara ya Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa iliyolenga kujionea utendaji wao katika kukusanya takwimu za utafiti huo.
Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akisisitiza jambo kwa watendaji wa Ofisi yake wakati wa ziara yake katika kijiji cha Isangha wilayani Bahi mkoani Dodoma iliyolenga kujionea utendaji wa wadadisi wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mkazi wa Kijiji cha Isangha wilayani Bahi mkoani Dodoma Bw. Robert Maswaga akisisitiza jambo kwa mdadisi wa Sensa ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Bw. Abdurahim Simba Anayeshuhudia ni Mtakwimu mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa. (Picha zote na MAELEZO)
Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa matokeo ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/2020 ni muhimu kwa kuwa mbali ya kuonesha mafanikio lakini pia yatabainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hivyo kuiwezesha Serikali kupanga na mikakati ya kutatua changamoto hizo.
Dr. Chuwa amesema hayo jana Agosti 14, 2020 huko katika kijiji cha Isang’ha wilayani Bahi mkoani Dodoma alipotembelea kufuatilia utendaji kazi wa wadadisi wa sensa hiyo Agosti 14, 2020.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutumia takwimu rasmi katika kupanga mipango ya maendeleo hivyo Sensa hiyo inafanyika wakati muafaka wakati Taifa likielekeza nguvu zake katika kujenga na kuimarisha sekta ya viwanda.
“Nimeridhishwa na kazi inavyoendelea katika ukusanyaji takwimu za Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma; sekta hii ni muhimu sana katika kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa nchi ambapo sekta ya Kilimo pekee inaajiri watanzania zaidi ya asilimia 67”, Alisisitiza Dkt. Chuwa.
Akifafanua amesema kuwa Sensa hiyo inafanyika kwa kuzingatia miongozo ya Kimataifa ili kuwezesha kupatikana kwa takwimu rasmi na zinazotambulika kimataifa na zitakazosaidia kuchochea maendeleo ikiwemo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.Aliongeza kuwa kazi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ni kuwaeleza wananchi yale yaliyotekelezwa kupitia Sensa na tafiti zinazofanyika ambazo ni chachu ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia utendaji wa wadadisi wa Utafiti huo Dkt. Chuwa amesema kuwa ameridhishwa na namna wanavyotekeleza majukumu yao na kuwataka kuzingatia sheria, taratibu, kanuni pamoja na mila na desturi wanapotekeleza jukumu la kukusanya takwimu katika maeneo waliyopangiwa.
“Kwa mujibu wa Sensa kama hiyo iliyopita, Tanzania kwa ina mifugo takribani milioni 32 hivyo Sensa inayofanyika sasa itawezesha Serikali kubaini changamoto na fursa zilizopo na kuweka mikakati ya pamoja katika kukuza sekta ya viwanda na biashara kwa maslahi ya wananchi,” Alisisitiza Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wadadisi wanapofika katika maeneo yao kwa ajili ya kukusanya takwimu.Kwa upande wao, wadadisi wa Sensa hiyo akiwemo Bi Hadija Yunus amesema kuwa wananchi wanatoa ushirikiano unaowawezesha kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Aliongeza kuwa takwimu wanazokusanya zitasaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.Naye mmoja wa wananchi wa kijiji hicho Bw. Jonas Mnyaturu amesema Sensa hiyo itawasaidia wananchi kuboresha ufugaji kwa kuwa Serikali itaweza kupanga mipango sahihi kwa kuzingatia takwimu zitakazokusanywa.
Aliongeza kuwa takwimu hizo zitawezesha kukuza pia sekta ya kilimo na kuiwezesha kuongeza tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo wa 2019/2020 ambayo ni ya tano kufanyika tangu Uhuru, inafanyika katika maeneo takribani 320 kote nchini.Kwa mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2007/2008 na uliwezesha Serikali kupanga mipango ya kukuza sekta hizo katika kipindi cha Miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment