Monday, January 3, 2022
SIREFA MBIONI KUANZISHA ‘MAJIMBO CUP’
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Hamisi Kitila (wa tano kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa kawaida wa mwaka uliofanyika mkoani Singida mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Hamisi Kitila akizungumza kwenye mkutano huo.
Kikao kikiendelea.
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida | CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA) kwa kushirikiana na vyama vya wilaya kupitia wabunge wa majimbo mbalimbali kipo mbioni kuanzisha ligi ya majimbo yaani ‘Majimbo Cup’ ambayo itakutanisha timu mbalimbali kutoka ndani ya majimbo mbalimbali ya kiuchaguzi yaliyopo mkoani hapa.
Kwa mujibu wa chama hicho ligi hiyo inatarajiwa kudhaminiwa na wabunge wa majimbo husika chini ya uratibu wa vyama vya michezo kupitia SIREFA, na michuano yake inatarajiwa kuwa ya ushindani kimajimbo na baadaye jimbo kwa jimbo kwa timu zitakazofanya vizuri.
Pia chama hicho pamoja na mambo mengine, kinatarajia ifikapo Januari 29 mwaka huu kuanza kuendesha ‘Ligi ya Soka la Wanawake’ itakayokutanisha makundi mbalimbali ya wanawake kutoka wilaya zote ndani ya mkoa wa Singida.
Akizungumza jana baada ya kumalizika kwa mkutano wa kikatiba wa kawaida ulioitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 23 ya Katiba ya SIREFA, Katibu Mkuu wa chama hicho Juma Mwendwa alisema moja ya vipaumbele vikubwa kwa mwaka huu ni kuhakikisha mapema iwezekanavyo wanafanikisha mipango yote iliyopo ili kunyanyua hadhi ya soka kwa makundi mbalimbali ndani ya mkoa.
“Kupitia mkutano huu tumeagiza vyama vya wilaya kufanya vikao vya kichama na kikatiba kuhakikisha wanacheza mashindano yote ya kikanuni na yasiyo ya kikanuni, kuanzisha michuano ya majimbo kwa kushirikiana na wabunge wa majimbo husika, lakini pia kuanzisha ligi ya wanawake sambamba na kuendesha mafunzo kwa makocha na waamuzi,” alisema Mwendwa.
Pia wajumbe kwa pamoja walijadili waraka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF ulioelekeza vyama vya soka vya Wilaya ya Singida Mjini SIDIFA na kile cha Singida Vijijini SIRUFA kuhakikisha vinakutana na kuanza mchakato wa kuungana na kutengeneza chama kimoja chenye katiba na jina la pamoja kwa wilaya ya Singida na sio vinginevyo.
Waraka huo wa TFF umeelekeza endapo kuna wilaya moja yenye halmashauri mbili kama ilivyo kwa sasa yaani-Halmashauri ya Wilaya ya Singida na Manispaa ya Singida basi kinapaswa kuundwa chama kimoja pekee cha soka na sio viwili (SIDIFA na SIRUFA)kama ilivyo kwa sasa.
Mwendwa alisema pia mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili taarifa iliyosheheni utekelezaji wa shughuli zote za chama hicho kwa mwaka uliopita-haliilivyokwasasa-na kuweka mipango madhubuti kwa mwaka unaoanza kwa ustawi wa SIREFA kwa mujibu wa katiba.
Zaidi kupitia mkutano huo wajumbe walipata fursa ya kufanya uchaguzi mdogo kwa lengo la kujaza nafasi 4 zilizokuwa wazi kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ya Mwekahazina na Wajumbe 3 wa Kamati ya Utendaji ndani ya chama hicho.
“Uchaguzi huu umefanyika na viongozi wamepatikana…ambapo Charles Chimwaga amechaguliwa kwa nafasi ya Mwekahazina, na wajumbe ni Shaban Mselem na Nyakalaga Waziri isipokuwa nafasi moja ya mjumbe haikufanikiwa kujazwa,” alisema Mwendwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment