Sunday, May 5, 2024
Absa Dar City Marathon 2024 zatimua vumbi jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Aron Luhanga (kushoto), akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za nusu marathon (Km 21) za Absa Dar City Marathon kwa upande wa wanaume, Dickson Paul kutoka Mwanza, mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Absa, Bi. Ndabu Lilian Swere.
*Benki ya Absa yaahidi kuendeleza udhamini wake
Na mwandishi wetu, Dar es Salaam
MBIO za Absa Dar City Marathon 2024 zimetimua vumbi lake jijini Dar es Salaam jana katika hali ya hewa ya utulivu mara baada ya tishio la kimbunga Hidaya kupoteza uwezo wake Kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka husika hivyo kuwafanya wakimbiaji kufurahia mandhari nzuri za jiji mashuhuri la Tanzania.
Ikiwa ni mara ya nne kufanya mbio hizi chini ya udhamini mkuu wa Benki ya Absa Tanzania, mtifuano huo ulishuhudia wanariadha zaidi ya 3000 wakifukuza upepo katika mitaa ya katikati ya Jiji hilo katika mbio hizo ambazo licha ya lengo lake kuu kuwa ni kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya Wodi ya wanawake ya Hospitali ya Mnazi Mmoja, lakini lingine ilikuwa ni kutangaza vivutio vya utalii vipatikanavyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kufanyika mbio hizo, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Aron Luhanga alisema kutokana na mafanikio ya mbio hizo, Benki Yao itaendelea kuwepo kwa kipindi kirefu katika kudhamini mbio hizo.
“Kama ahadi ya chapa yetu isemayo Tunadhamini Story Yako, Benki ya Absa itaendelea kuthamini story za maisha ya watanzania, kwani sehemu ya mapato ya mbio hizi yatakwenda kusaidia jamii kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya wanawake na watoto.
“Absa tunaamini kuwa mtu yoyote anaweza kuandika story yake kutokana na mazoezi na kukimbia ni moja ya mazoezi, lakini pia tunaamini utajiri upo kwenye afya, na kukimbia kunaleta afya, hivyo jamii na nchini itapiga hatua kubwa ya kimaendeleo kukiwa na watu wenye afya Bora,Absa tupo kihakikisha Story hizo zinaandikwa kwa ufanisi” alisema Bwana Luhanga.
Akizungumza kuhusu huduma zao za kibenki Bwana Luhanga alisema benki yao imesheheni bidhaa na huduma mbalimbali zenye ubora wa kamataifa ikiwa ni pamoja na akaunti za watoto, mikopo ya nyumba, magari pamoja huduma ya kadi ya mkopo (credit card) ya kipekee nchini kabisa inayomwezesha mteja kupata kadi huyo ikiwa tayari imewekewa kiasi cha pesa cha kuanzia.
Naye Mwenyekiti wa The Runners Club, waandaaji wa Absa Dar City Marathon, Godfrey Mindu aliishukuru Benki ya Absa pamoja na wadhamini wengine kwani kujitoa kwao kunaenda kuleta mabadiliko makubwa kwa maisha ya watanzania.
Dar City Marathon 2024 ilishirikisha mbio za KM 5, 10 na 21 huku kwa upande wa KM 10 wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Anastasia Dolomongo kutoka Arusha akitumia muda wa DK 34:04:31, kwa upande wa wanaume mshindi alikuwa Emanuel Shahanga kutoka Hanang akitumia muda wa Dk 29:00:03.
Kwa upande wa mbio za KM 21 za nusu marathon upande wa wanawake, ushindi wa kwanza ulienda kwa Sara Ramadhani kutoka Arusha pia akitumia muda wa Saa 1:13:21:08, huku kwa upande wa wanaume, Dikson Paul kutoka Mwanza akiibuka kidedea kwa kutumia muda wa Saa 1:02:58:04.
Mbali na Benki ya Absa kama mdhamini mkuu, wadhamini wengine ni Kampuni ya Alliance Life Assurance, Hill Water, Kilimanjaro Milk na Kampuni ya Garda Security.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Lilian Swere (kushoto), akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za nusu marathon (Km 21) za Absa Dar City Marathon kwa upande wa wanawake, Sara Ramadhani kutoka Arusha, mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki wa Absa, Bwana Aron Luhanga.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Lilian Swere (kushoto), akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa mbio za KM 10 za Absa Dar City Marathon kwa upande wa wanawake, Anastasia Dolomongo kutoka Arusha, mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki wa Absa, Bwana Aron Luhanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment