Thursday, August 10, 2017
COKE STUDIO AFRIKA YACHANGIA KUPAISHA KAZI ZA WASANII NCHINI TANZANIA
Onyesho maarufu la muziki la Coke Studio
Africa, ambalo hivi sasa limeingia katika awamu ya tano chini ya udhamini wa
kampuni ya Coca-Cola, limechangia kwa kiasi kikubwa kutangaza wasanii wa
Tanzania waliofanikiwa kushiriki na kazi zao nje ya nchi hususani wanaopiga muziki
wa Bongo Fleva.
Kazi za wasanii zimejulikana kutokana na
mtindo unaotumika katika onyesho hili la kuwakutanisha wasanii nguli kutoka
nchi mbalimbali za Afrika ambapo hufanya kolabo za pamoja ambazo zinarushwa
kupitia vituo vya luninga na kufuatiliwa na wapenzi wengi wa muziki kupitia
mitandao ya kijamii.
Baadhi ya wasanii kutoka Tanzania ambao
wameshiriki onyesho hili tangu lianzishwe ni Lady Jaydee, Diamond Platnumz,
Vanessa Mdee, Alikiba, Joh Makini, Shaa, Fid Q, Ben Pol, Nahreel na msimu huu
wa tano wapo Rayvanny, Izzo Bizness na Nandy.
Misimu minne iliyopita ya Coke Studio Africa
imekuwa na mafanikio makubwa katika kuutangaza muziki wa Bongo Fleva barani
Afrika. Wamejiongezea mashabiki, wamejifunza mambo mbalimbali kuhusu muziki
kama burudani, muziki kama taaluma na muziki kama biashara na tena si tu kutoka
kwa wasanii wenzao wa Afrika na Marekani
Vilevile wasanii wote ambao wamepita kwenye
onyesho hili wameendelea kupata mafanikio makubwa ya kimuziki kutokana na kazi
zao kuendelea kutamba na kukubalika kwa wengi ndani na nje ya Tanzania.
Taarifa kutoka kampuni ya Coca-Cola
iliyotolewa hivi karibuni imeeleza kuwa onyesho la Coke Studio Africa, ambalo
umaarufu wake umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka msimu huu utakuwa na
burudani za aina yake kutoka kolabo za wasanii nguli barani Afrika kuanzia
Afrika Magharibi mpaka Afrika ya Kusini na litarushwa na vituo vya luninga kwenye
nchi zaidi ya 30 barani Afrika.
Tangia onyesho hili lianzishwe limekuwa kiungo
kikubwa cha kuwakutanisha wanamuziki wa Afrika kufanya kazi kwa pamoja na
kupiga muziki wenye vionjo kutoka sehemu mbalimbali za Afrika ikiwemo kuleta
burudani kubwa kwa washabiki wa muziki wa kiafrika na kuwaunganisha waafrika hususani
vijana kupitia muziki.
Katika msimu wa Coke Studio Africa unaotarajia
kuanza kurushwa kwenye luninga mapema mwezi ujao unashirikisha wasanii kutoka
katika nchi za Kenya, Afrika ya Kusini, Uganda, Tanzania, Rwanda, Ethiopia,
Nigeria, Ghana, Angola, Zimbabwe, Togo, Cote d’Ivoire, Madagascar, Mauritius,
Msumbiji, DRC na Cameroon.
Tags
# SPORTS AND ENTERTAINMENT
Share This
SPORTS AND ENTERTAINMENT
Labels:
SPORTS AND ENTERTAINMENT
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment