Wednesday, November 15, 2017
Historia, maisha na mafanikio ya soka la Ndikumana Afrika na Ulaya
Jumatano November 15, 2017 Soka la Afrika Mashariki limepokea taarifa za simanzi kufuatia kifo cha mchezaji wa zamani Hamad Ndikumana ambaye hadi anafikwa na mauti alikuwa akihudumu kama kocha msaidizi wa klabu ya Rayon Sports ya Rwanda.
Kifo cha Ndikumana kinaelezwa kusababishwa na matatizo ya moyo lakini hadi sasa bado taarifa za kitabibu hazijatufikia ambazo zinafafanua kwa kina sababu iliyopelekea kifo cha nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Rwanda.
Watu wengine wanachanganya kati ya Hamad Ndikumana na Selemani Ndikumana, Selemani ni mzaliwa wa Bujumbura Burundi na aliwahi kucheza soka kwenye klabu ya Simba kati ya mwaka 2006-2007, hawa ni watu wawili tofauti kabisa.
Sifa kubwa ya Ndikumana kwenye soka
Alisifika kwa uwezo wake mkubwa wa kufanya tackling, ndio ulikuwa utambulisho wake ukimuuliza mtu yeyote aliyemfahamu vyema Ndikumana lazima atakugusia kuhusu hilo.
Historia fupi ya masiha ya Hamad Ndikumana
Hamad Ndikumana maarufu kwa jina la ‘Katouti’ alizaliwa October 5, 1978 (39) Kigali, Rwanda. Alikuwa na urefu wa mita 1.81 ambazo ni sawa na futi 5 na inchi 11, alikuwa na uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni (kulia na kushoto).
Alianza kucheza soka la ushindani mwaka 1998 akiwa na klabu ya Rayon Sports FC ya nyumbani kwao Rwanda ambapo alidumu kwa msimu mmoja tu (1998-99) kabla ya kutimkia Ulaya kucheza soka la kulipwa.
Ndikumana kama Samatta tu
Mwaka 2000 alijiunga na klabu ya K.F.C. Turnhout ya Ubelgiji taifa ambalo nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta ameanzia kucheza soka barani Ulaya akiwa na klabu ya KRC Genk.
Amecheza Ubelgiji kwa miaka mitano (2000-2005) akiwa na vilabu vine tofauti ambavyo ni K.F.C. Turnhout 2000-2001, RSC Anderlecht 2001-2002, KV Mechelen 2002-2003, KAA Ghent (Ubelgiji) 2003-2005.
Maisha mapya Cyprus
Mwaka 2006 Ndikumana aliondoka nchini Ubelgiji na kuelekea zake Cyprus ambako pia aliendelea kucheza soka hadi mwaka 2011, akiwa Cyprus alicheza katika vilabu sita kwa misimu sita tofauti (2006-2011).
Vilabu ambavyo amecheza Ndikumana akiwa Cyprus ni APOP Kinyras Peyias 2005-2006, Nea Salamis Famagusta FC 2006-2007, Αnorthosis Famagusta FC 2007-2008, AC Omonia 2008-2009, AEL Lemesou 2009-2010, APOP Kinyras Peyias 2011.
Atakumbukwa Rwanda na Afrika
Aliisaidia Rwanda kufuzu kucheza michuano ya mataifa ya Afrika mwaka 2004 ikiwa ni mara ya kwanza kwa The Amavubi kushiriki michuano hiyo katika historia ya soka la Rwanda kimataifa. Jina lake litaendelea kubaki kwenye vitabu vya soka la Rwanda na Afrika kutokana na kuwa miongoni mwa wachezaji walioshiriki AFCON 2014.
Ndikumana alikuwa shemeji yetu
July 2009 Ndikumana alifunga ndoa na mrembo Irene Uwoya ambaye ni staa wa Bongo movies, ndoa hiyo ilifungwa kwenye kanisa la Mt. Joseph Dar es Salaam Tanzania. Wawili hao walijaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume (Krish), baadaye ndoa yao ilivunjika na kila mmoja akaendelea na maisha yake.
Tags
# SPORTS AND ENTERTAINMENT
Share This
SPORTS AND ENTERTAINMENT
Labels:
SPORTS AND ENTERTAINMENT
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment