Friday, September 27, 2019
Watanzania milioni tano wasaidiwa kupata haki zao
Bw. Eugen Mawele (kushoto)-masaidizi wa Kisheria kutoka wilaya ya Chemba (Dodoma) akipokea cheti cha mafunzo rejea (re-fresher course) kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa LSF,Bi. Lulu Ng’wanakilala—wakati wa mkutano wa wadau wa huduma za msaada wa kisheria yalioandaliwa na shirika la Legal Services Facility (LSF) jijini Dodoma (Picha na Mpigapicha Wetu).
Zaidi ya watanzania milioni 5 maskini wamepatiwa msaada wa kisheria na kukwamuliwa kutoka katika matatizo mbalimbali ya kisheria chini ya mradi wa msaada wa kisheria unaofadhiliwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF).
Haya yalibainishwa hivi karibuni mjini Dodoma wakati wa mkutano wa mashirika yanayojishughulisha na utoaji wa msaada wa kisheria yanayotekeleza miradi ya msaada wa kisheria nchi nzima chini ya ufadhili wa LSF. Dhumuni kubwa la mkutano huu ni wayawezesha mashirika yapatayo 200 yanayotekeleza miradi ya LSF kujadili mafanikio yaliofikiwa na kuweka mikakati madhubuti itayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria—lengo kuu likiwa ni kuwakwamua mamilioni ya watanzania wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kisheria.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa mkutano, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Bi. Lulu Ng’wanakilala amesema “kwa ujumla, tumepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mradi huu...mpaka sasa, tumeshawafikia watu wenye matatizo mbalimbali ya kisheria zaidi ya milioni 5 tangu mradi uanze Mwaka 2011.”
“Na watu hawa wote wamamepatiwa msaada wa kisheria na elimu kuhusu maswala ya kisheria kupitia wasaidizi wa kisheria wanaotoka katika mashirika tunayoyafadhili nchi nzima.” Mpaka sasa, LSF imetengeneza wasaidizi wa kisheria takribani 3000, wanaosaidia watanzania, hasa waishio vijijini kupata msaada wa kisheria na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili hasa wanawake. Baadhi ya changamoto hizi ni za miradhi, ardhi, malezi kwa watoto, mimba za utotoni na nyingine nyingi.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa LSF, mkutano wa wadau, mbali na mambo mengine, umelenga kutoa nafasi kwa mashirika husika kufanya tathmini ya kina kama malengo ya mradi yamefikiwa au la, na kuweka mipango ya kupanua wigo wa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, lengo likiwa ni kuwawezesha watanzania maskini (wenye matatizo mbalimbali ya kisheria) kupata haki zao.
Taarifa iliyotolewa na LSF kwa vyombo vya habari inasema “huduma za msaada wa kisheria nchini zinakuwa kwa kasi na kuwanufaisha wengi, mfano mwaka jana zaidi ya watu milioni 3 walifikiwa kwa kupatiwa elimu ya maswala ya sheria, zaidi ya kesi 76,000 ziliwakilishwa kwa watoa huduma ambapo asilimia 60 za kesi hizo zilipatiwa usuluhisho.”
Marius Isavika, Meneja Mradi wa Shirika la KASODEFO (Mkoa wa Simiyu)-moja ya mashirika yanayotekeleza mradi wa LSF, amesema shirika hilo limefanikiwa kutatua migogoro mengi ya ardhi na matatizo mengine ya wananchi maskini wanaoshi vijijini kupitia wasaidizi wa kisheria walioka katika kata mbalimbali mkoani Simiyu.
“Tunaowalenga zaidi ni wanawake na maskini wanaoishi vijijini, hasa ukizingatia kuwa ni asilimia 7 tu ya wananchi wa Simiyu ndo wanaishi mjini, wengi wote wanaishi vijijini. Sisi, KASODEFO tunaona ujuo wa mradi wa LSF kama ukombozi mkubwa kwa maskini ( wenye matatizo ya kisheria) katika mkoa wetu wa Simuyu.”
Kwa upande wa Veronica Ollomi, Afisa Habari wa Shirika la KWIECO (Kilimanjaro), amesema kupitia wasaidizi wake wa kisheria wapatao 170, shirika limefanikiwa “kuwakwamua watu wengi kutoka katika matatizo mbalimbali ya kisheria, lakini bado tuna changamoto nyingi, kwa sababu wasaidizi wa kisheria tulionao wako katika kata chache, ukinganisha na watu waohitaji msaada wa kisheria, hivyo kufanya wengi wenye huitaji kukosa huduma hii.”
“Hata hivyo, kama shirika bado tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi, hasa katika kata ambazo hazina wasaidizi wa kisheria, ili kuwawezesha kutumia mifumo iliyopo—mabaraza ya kata, serikali za mitaa, afisa maendeleo wa jamii na vyombo mbalimbali--ili kuweza kupata haki zao.”
Aidha mkutano huo, ulilenga pia kujengeana uwezo, kuaangalia changamoto zinazozikumba jamii katika maeneo mbalimbali nchini na kuweka vipaumbele katikati utekelezaji ili kuleta maendeleo na matokeo tunayoyatarajia ambayo ni haki sawa kwa wote kwa maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla, amesema Bi. Scholastica Jullu, Mkurugenzi wa Mradi-LSF.
“Mkutano pia ulitoa nafasi kwa mfadhili wa miradi, LSF kueleza mipango mikakati yake inayolenga kuboresha huduma za usaidizi wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria mijini ambapo changamoto za mjini nitofauti na changamoto za vijijini ambapo LSF imekuwa ikitekeleza miradi yake maeneo ya vijijini zaidi,” imesema taarifa ya LSF.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania Yakamilisha Kampeni ya Kusisimua ya "Spend & Win" kwa Droo ya Mwisho na Hafla ya Kukabidhi Gari
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Ndabu Lilian Swere (kushoto), akihutubia hadhira wakati wa droo ya tatu y...
No comments:
Post a Comment