Monday, December 7, 2020
STAMICO YAPATA TUZO YA MFANYABIASHARA MSHIRIKA BORA, NCHINI INDONESIA
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse akiwa katikati akiwa ameshika tuzo ya Mfanyabiashara na Shirika Bora katika sekta ya madini zilizotolewa na Ubalozi wa Indonesia nchini ,jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Indonesia nchini akiwa katika picha ya Pamoja mara baada ya kutoa tuzo katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Picha ya Pamoja ya Balozi wa Indonesia akiwa baadhi ya walitunukiwa vyeti na Tuzo katika sekta ya madini katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kuchanja mbuga kimataifa baada ya kupata tuzo ya mfanyabiashara mshirika bora katika sekta ya madini kutoka nchi ya Indonesia kwa mwaka 2020.
Tuzo hiyo imetolewa na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Prof. Ratlan Pardede katika hafla ya kutambua na kuthamini mchango wa wafanyabiashara washirika wa nchi ya Indonesia iliyofanyika katika ofisi za ubalozi wa Indonesia zilizopo jijini Dar es salaam.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse ameushukuru ubalozi wa Indonesia kwa kutambua mchango wa shirika katika uwekezaji kwenye sekta ya madini na kusema kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kimaendeleo na ishara ya mabadiliko ya STAMICO katika kujiendesha kibiashara na kujitanua kimataifa.
Dkt.Mwasse alisema STAMICO imekuwa na ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu baina yake na Shirika la Madini la Indonesia lijulikanalo kama PT.Timah, ushirikiano huo umepelekea kusaini hati ya makubaliano katika kuendeleza sekta ya madini kupitia miradi mbalimbali hususani ya madini ya bati yaliyopo wilayani Kyerwa.
Ushirikiano huo umefungua milango ya wataalamu wa madini kutoka Shirika hilo la madini kuja nchini kujionea maeneo ya uwekezaji na kufanikiwa kuchukua sampuli za madini ya bati na dhahabu na kuyapeleka katika maabara ya madini iliyo chini ya wakala wa jiolojia na utafiti GST jijini Dodoma ili kuweza kujiridhisha zaidi.
Katika kuendeleza ushirikiano huo Balozi wa Indonesia Prof. Dkt. Ratlan Pardede ameishukuru STAMICO kwa hatua ya kusaini hati ya makubaliano na kutoa ushirikiano mkubwa wa kitaalamu kwa wawekezaji waliokuja nchini na kuwapeleka katika maeneo mbalimbali ya miradi.
Aidha, ameipongeza STAMICO chini ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wake Dkt. Mwasse kwa jitihada zake za dhati za kuendeleza mawasiliano na taasisi ya PT.Timah licha ya kuwepo kwa changamoto ya ugonjwa wa Covid19 ambao ulitikisa dunia.
Alisema hii ni dhamira ya dhati inayodhihirisha nia ya Shirika hilo katika kuwavutia wawekezaji kwenye sekta ya madini.
Alisema STAMICO imetunukiwa tuzo hiyo miongoni wa taasisi nne zikiwemo ambazo zimetoa mchango na ushirikano mkubwa kwa wawekezaji kutoka nchini Indonesia.
“Tuzo hii kwa STAMICO ni ishara kuwa Shirika limeanza kufungua milango ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, kwa kuwaunganisha wawekezaji na wachimbaji wadogo ili kuweza kuboresha shughuli na kuinua sekta ya uchimbaji mdogo ambayo kwa muda mrefu imeonekana ni sekta duni.” alisema.
Aidha, aliahidi kuendelea kufanya kazi na STAMICO bega kwa bega ili kuboresha sekta ya madini nchini na kutoa mwaliko kwa wataalamu wa STAMICO kutembelea taasisi za madini zilizopo nchini indonesia ili kupata uzoefu utakaoleta chachu ya mabadiliko katika sekta hiyo.
Akizungumzia malengo ya baadaye Dk. Mwasse ameongeza kuwa bado kuna mikakati mingi inayoiunganisha STAMICO na nchi ya Indonesia ikiwemo biashara ya madini ya bati inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
“Kuna mpango wa kufanya ziara ya wataalamu katika taasisi ya PT.Timah iliyopo nchini Indonesia kufuatia mwaliko walioupata tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwenda kujionea na kujifunza kwa vitendo namna Indonesia inavyofanya kazi katika sekta ya madini.
“Pia tutaimarisha mradi wa madini ya bati ili kuboresha soko la madini hayo litakalochochea kukua kwa uchimbaji wa madini ya bati na kubora hali ya Maisha ya wachimbaji wadogo,” alisema.
Aidha, Alisema imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dk. John Magufuli za kuboresha na kuendeleza uwekezaji nchini kwa kuhakikisha wawekezaji wanapewa ushirikiano na kupata taarifa zinazohusika
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment