Sunday, November 28, 2021
JUKWAA LA WANAWAKE LITUMIKE KULETA MAENDELEO - MABULA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wanawake wa mkoa wa Shinyanga wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani humo mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko.
Baadhi ya Madiwani Wanawake wa mkoa wa Shinyanga wakiwa katika Mkutano wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani humo mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza katika mkutano wa Jukwaa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi mkoani Shinyanga lililofanyika mwishoni mwa wiki.
Sehemu ya washiriki wa mkutano wa Jukwaa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi mkoani Shinyanga lililofanyika mwishoni mwa wiki.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hatimiliki ya ardhi Bi Nasra Yusufu Katopola mkazi wa Ngokolo Manispaa ya Shinyanga wakati wa ziara ya siku mbili mkoani Shinyanga mwishoni mwa wiki.
Na Munir Shemweta, WANMM SHINYANGA | Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Shinyanga kutumika kama nyenzo ya kuwaletea maendekeo sambamba na kuwahamasisha wanawake kuwa na umiliki wa ardhi.
Akizungumza na wanawake wa jukwaa hilo kutoka kata 17 za mkoa wa Shinyanga mwishoni mwa wiki mkoani humo, Dkt Mabula alisema kiu yake ni kuona majukwaa ya wanawake nchini yanafanya kazi ya kuwawezesha wanawake ikiwemo kumiliki ardhi hasa ikizingatiwa kuwa mwanamke ni nguzo ya maendeleo.
“Tunachotaka sasa kama wanawake hatuwaachi nyuma wanaume lakini na sisi lazima tujiimarishe kiuchumi maana tumekuwa wasindikizaji kwa muda mrefu, tunataka kubadilisha ni kama tumechelewa” alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi mwanamke akikamata uchumi maendeleo lazima yatakuwepo na kwa muda mrefu mwanamke amebaki nyuma wakati anaweza kufanya mambo makubwa na kuwataka wanawake kutoigana kwenye vitu vitakavyowashinda kuvisimamia.
Aidha, aliwataka wanawake hao wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Shinyanga kusimamia yale mambo waliyokubaliana na kuongeza kuwa, jukwaa lisipojiandaa katika shughuli zake itakuwa ngumu kufanikiwa.
“Kuna fursa katika maeneo yetu na tunahitaji mitaji mikubwa na tuwe na miradi itakayokuwa vielelezo na tusiende ili mradi tu bali tuwe na shughuli kubwa za uzalishaji mali, Roma haikujengwa kwa siku moja” alisema Dkt Mabula.
Akigeukia umiliki wa ardhi kwa wanawake, Naibu Waziri Dkt Mabula aliwataka wanawake kuanza kujitokeza kuomba umiliki wa ardhi hasa kwenye maeneo mapya sambamba na kuhakikisha ardhi wanayoipata iwe imepimwa. Aliwaambia kuwa, sheria ya ardhi haizuii mwanamke kumiliki ardhi hivyo wachangamkie kupata ardhi katika maeneo mapya ya mkoa huo inapopita miradi ya kimkakati.
"kwa sasa sisi wanawake lazima tubebe umiliki wa ardhi na kuitumia kijiletea maendeleo kama vile kuchukulia mikopo katika mabenki” alisema Naibu Waziri Mabula.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko aliwataka wanawake wa mkoa huo kuanza michakato ya kuhakikisha nao wanamiliki ardhi ili kujiletea maendeleo.
“Ninawaomba wanawake wenzangu tuanze kutumia fursa kwa kumiliki ardhi na tumapopata fedha katika shughuli zetu tuhakikisha tunazitunza ili tujiletee maendeleo” alisema Mboneko.
Mkutano huo wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoa wa Shinyanga limeshirikisha Wajasiriamali kutoka kata za Mjini, Kambarage, Lubaga, Kitangili, Ngokolo, Ndendezi, Ibadakuli, Kolandoto, Old Shinyanga, Chide, Chamaguha, Ndala, Masekelo, Mawaza, Mwamalili na Kizumbi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment