Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi katika taasisi tatu tofauti nchini.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu, ilisema Rais amemteua Dk Baghayo Saqware kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Dk. Saqware ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), aliwahi kuongoza taasisi hiyo kwa mafanikio lakini aliondolewa na Rais wa Serikali ya awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli.
Baadhi ya mafanikio aliyoyapata ni kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia tozo za kibima kutoka sh. Bilioni 10.1 mwaka 2015 hadi sh bilioni 12.1 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 11;
Mafanikio mengine ni kuzuia ubadhirifu kwa kuimarisha mfumo wa kieletroniki wa TIRA MIS wenye kuzuia na kuhakiki bima zote za magari nchini. Hatua hii imesaidia kupunguza ubadhirifu na kuwalinda watumiaji wa huduma za bima ya magari na vyombo vingine vya moto.
Mafanikio mengine ni kupanua wigo wa utoaji huduma za bima kwa kuanzisha na kutekelezwa kwa kanuni za kusimamia huduma za bima kupitia mabenki (Bancassurance Regulations 2019) ambazo zilipitishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philipo Mpango wakati huo Machi 2019.
Kanuni hizi zimelenga kuongeza upatikaji wa huduma za bima nchini kwa urahisi na ufanisi kupitia mtandao wa matawi ya benki Tanzania. Utekelezaji huu ulileta uhasama baina ya Kamishna wa Bima na madalali wa bima (Insurance Brokers) ambao waliamini uanzishwaji wa kanuni hizi zinalengo la kuua biashara ya udalali, jambo ambalo si sahihi.
Kuondoa kero kwa wateja na wafanyabiashara ya bima ni moja ya mafanikio wakati ule baada ya kutekeleza kwa vitendo mabadiliko ya sheria namba 10 ya mwaka 2009 kifungu namba 72 kinachoelekeza ada za bima kulipwa moja kwa moja kwa kampuni ya bima bila kupitia kwa mtu wa kati (insurance intermediaries).
Mafanikio mengine ni kuthibiti utoroshwaji wa tozo za bima kwa kuanzisha utaratibu wa ithibati (“accreditation”) kwa makampuni na madalali wa nje ya nchi wanaofanya biashara ya bima mtawanyo na kampuni zilizosajiliwa nchini.
Mengine ni kuongeza uwezo wa kubakiza tozo nchini (Retention Level) kulinda wateja wa bima kwa mfumo bora wa malipo ya fidia, kulinda ajira za Watanzania, kuweka utaratibu wa kuratibu wataalamu bima nchini.
Mbali na Dk Saqware, Rais Samia pia amemteua Charles Itembe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Eneo Maalumu la Mauzo ya Nje (EPZA). Itembe ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Samia pia amemteua Ernest Mchanga kuwa Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC).
Mchanga ni Katibu Msaidizi, Fedha na Utawala, Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC) kutoka Wizara ya Fedha na Mipango. Uteuzi huo ulianza Januari mosi mwaka huu
Tuesday, January 4, 2022
RAIS SAMIA ATEUA WATATU SAQWARE AREJESHWA TIRA
Rais Samia Suluhu Hassan.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Benki ya Absa Tanzania kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu
Meneja Huduma za Jamii wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Abigail Lukuvi (wa pili kushoto), Mwanafunzi wa Shule ya Uhuru Mchanganyiko, Crispian ...
No comments:
Post a Comment